Soko liko wapi

Soko liko wapi
Soko la Mazao ya wakulima ndiyo changamoto kubwa huko vijijini. Wakulima wakisubiri wateja kando ya barabara ya Morogoro-Dodoma eneo la Gairo ili wanunue viazi vitamu

Special News Pages

Tuesday, July 6, 2010

Food Security/ Cooperative Unions

TASAF YAPAMBANA NA NJAA MASASI

Julai, 4, 2010

Na Hassan Simba, Masasi

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji kumi vya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara unatarajia kutekeleza mradi wa uhakika wa chakula kwa kaya duni utakaogharimu zaidi ya sh. Milioni 400 kwa mwaka huu wa fedha wa serikali.

Mratibu wa mfuko huo wilayani Masasi, Neema Joseph amebainisha hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa yaliyofanyika kiwilaya mji mdogo wa Ndanda uliopo kata ya Mwena na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi waliopata fursa ya kuuliza maswali na kupata majibu ya papo kwa hapo.

Mratibu huyo alimwambia mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Juma Satima ambaye ni makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo alipotembelea banda hilo la maonesho kuwa kwa mwaka huu wa fedha wa serikali 2010/11 mfuko huo umejidhatiti kukabiliana na tatizo la njaa wilayani humo.

“Miradi 20 itatekelezwa katika mradi huu…..kumi ni ya vikundi na mingine ni ya jamii…katika hii miradi ya jamii mfuko unatarajia kutumia sh. Milioni 300, ikiwa kila mradi utagharimu sh. Milioni 30, miradi ya vikundi itakuwa kumi na kila mmoja utagharimu sh. Milioni kumi” alisema Joseph

Alifafanua kuwa miradi hiyo inawalenga wananchi wenye hali duni ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na hatimaye kuwaondoa katika tatizo la kukumbwa na njaa kila mwaka ambalo limekuwa likichangia kukua kwa umasikini katika kaya hizo.

Alivitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kuwa ni Mrunderunde na Mumbaka kata ya Marika, vijiji vya Mchoti, Utimbe na Mbangala kata ya Lipumburu, Mwongozo, Mkungu na Nangoo kata ya Nanganga wakati kata ya Mkundi ni vijiji vya Chikolopola na Majembe.

Akihutubia katika maadhimisho hayo Satima alisema halmashauri yake imepiga hatua katika kuwahudumia wananchi wake kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa wito kwao kuwa tayari kuchangia nguvu kazi katika kutekeleza miradi hiyo.

“Kwa mwaka 2009/2010 halmashauri ilikadria kutumia jumla ya sh. Milioni 19.7 kwa ajili ya mishahara, na matumizi mengine ikiwemo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo….hadi mwezi Mei, matumizi halisi yalikuwa sh. Milioni 13 sawa na asilimia 66.07 ya lengo” alisema Satima

Mwisho



VYAMA 32 KUFIKISHWA MAHAKAMANI TANDAHIMBA
Na Hassa Simba, Tandahimba.

VIONGOZI wa vyama 32 vya msingi vya ushirika wa kilimo na masoko vya wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara vinatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwaibia wakulima wa korosho katika maeneo yao .

Habari zinasema kuwa tayari mwanasheria wa halmashauri ya wilaya hiyo, Menace Ndoroma ndiye ameshakabidhiwa jukumu la kuhakikisha viongozi hao wanapandushwa kizimbani kujibu tuhuma za ubadhilifu wa mamilioni ya shilingi ya wakulima wa korosho katika maeneo yao .

Viongozi hao wanadaiwa kunufaisha visivyo halali fedha za wakulima waliouza korosho katika vyama vyao hivyo kusababisha washindwe kulipa malipo ya tatu kama walivyoelekezwa na serikali mkoani Mtwara.

Ndoroma alikithibitishia kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo kilichoketi mwishoni mwa wiki mjini Tandahimba kuwa mchakato wa kuwafikisha mahakamani viongozi hao upo mbioni kukamilika na kwamba wale wote waliohusika na ubadhilifu huo watakutana na mikono ya sheria.

“Suala la viongozi wa vyama vya msingi 32 kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuwaibia wakulima lipo mbioni kukamilika……naomba kikao kisitumie muda kujadili hili” alisema Ndoroma

Awali ofisa ushirika wa hamlmashauri ya wilaya hiyo, Saidi Munjai akisoma taarifa ya hali ya ununuzi wa korosho kwa msimu 2009/10 hadi kufikia Juni, alibainisha kuwa malipo ya tatu yamezua tafrani na mgogoro mkubwa baina ya wakulima na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika kutokana na wakulima kutoolipwa haki zao stahiki

Munjai alikieleza kikao hicho kuwa kati ya vyama vya msingi vya ushirika 64 vya wilayani humo, vyama 32 havijakamilisha malipo ya tatu wakati chama kimmoja hakijalipa kabisa malipo hayo, tukio hililoambatana na vurugu kwa wananchi kuwafungia ghalani viongozi wa vyama hivyo na kuhatarisha amani wilayani humo.

“Msimu wa ununuzi wa kotosho uliambatana na vurugu wakati wa malipo ya tatu kutokana na vyma vya msingi kulipa malipo magodo kuliko ambayo walistahili kulipa….hadi sasa licha ya serikali kuagiza kufanyika kwa malipo haraka iwezekanavyo bado vyama hivyo havijatekeleza agizo hilo ” alisema Munjai

Wakichangia hoja hiyo wajumbe wa kikao hicho walishauri viongozi hao kupandishwa kizimbani haraka iwezekanavyo kabla ya kuanza kwa msimu mwingine ili kuhakikisha wakulima wanapata haki zao.

“Hili suala liendane na utekelezaji wake ……wasipofikishwa mahakani haraka msimu mwingine wa korosho utawakuta viongozi hao na kutengeneza mazingira ya kuzidi kuwaibia wakulima wetu” alisema Jaffari Mwadili katibu wa Chadema wa wilaya hiyo.



Mwisho

No comments:

Post a Comment